Mapambano kati ya ubepari na ujamaa nchini Kenya yana historia ndefu. Lakini hayakuwa mapambano yaliyo sawa, kwani ukoloni ulikuwa tayari umeanzisha ubepari kwa nguvu tangia siku za awali. Na bado, ubepari haukuweza kukidhi mahitaji ya watu, kama inavyodhibitishwa na kushindwa kwake katika nchi zote za kibepari barani Afrika. Ujamaa pekee ndio ungeweza kukidhi matakwa ya wananchi ya ardhi, uhuru, haki na usawa kama ilivyopangwa, kwa mfano, na Muungano wa Watu wa Kenya (KPU) ambao kauli mbiu yake ilikuwa ‘Uhuru na Ujamaa’. Azimio la Wananchi la KPU (1969, 6) lilitaja sera zake kwa uwazi:
Jawabu lipo kwenye mfumo unaojulikana kama Usosholisti. Kwa maana, kitu cha kwanza muhimu ili kuwe na mgawanyo wa haki katika jamii maskini ni kuweka nguvu za kiuchumi mikononi mwa watu. Hili halifanywi tu kwa kuwaweka Waafrika wachache kama wakurugenzi wa makampuni makubwa, na kugawa maeneo makubwa ya ardhi kwa Mawaziri na mahusiano wao… jibu lilikuwa katika kuweka msingi wa kubadilisha muundo wa uchumi na uwezo wa serikali ya Afrika ndani yake ili maendeleo yetu yasiwe tena katika huruma ya mabepari wa kigeni au wa ndani.
Manifesto hiyo inatoa kauli ya wazi kwamba ‘Serikali ya KPU itasimamia uchumi kulingana na kanuni za usosholisti’. Lakini ubepari ulivyozidi kujikita, ndivyo chaguo pekee la watu likawa ni kuupinga. Mzozo mkuu katika jamii ulikuwa kati ya wafanyikazi waliokuwa wakidai ardhi, uhuru na haki kwa ukinzano na mabepari wakala waliodai haki yao’ ya kudhibiti na kumiliki mali na rasilimali’ za taifa. Katika vita hivi, tabaka tawala la wachache, ambalo liliunga mkono ubepari, lilipata mamlaka na uwezo ilhali watu wengi wakiwemo wafanyikazi wakapoteza. Je, hili liliwezekanaje, wakati nguvu za watu wanaofanya kazi zilishinda Milki ya Uingereza na kuhakikisha uhuru? Kama podikasti ya Sheng’ Hadi Kila Mtu Awe Huru (2021) inavyouliza, ‘Nchi ya Kenya ilifanikiwaje kuwa huru…bila watu wa Kenya kupata uhuru?’
Jambo hili linaweza kuelezewa kwa kuzingatia kipengele muhimu cha ubepari: unagawanya watu kwa matabaka pinzani ambapo tabaka tawala hudhibiti mamlaka ya serikali ili kujitajirisha yenyewe kwa gharama ya watu wengi. Bado sababu nyingine inayoelezea kujimudu kwa wachache madarakani ni msaada wa fedha za kimataifa, biashara, maslahi ya kisiasa na kijeshi.
Mgawanyiko wa jamii kwa msingi wa tabaka pinzani unasababisha kuwepo kwa tabaka la wafanyikazi na upinzani wake kwa ubepari. Ni mzunguko huu wa ukandamizaji wa ubepari kwa upande mmoja, na upinzani wake kutoka kwa watu kwa upande mwingine, ndio sifa kuu ya hali ya zamani na sasa nchini Kenya.
Matukio ya sasa na historia nchini Kenya mara nyingi huonekana katika vitendo vya mtu binafsi na kikundi kuhusiana na masuala ya siasa, sheria, utawala na viongozi. Kisichoonekana au kudhihirika ni itikadi inayosimamia vitendo hivi. Rekodi za kihistoria za Kenya zinaonyesha kile viongozi na vyama vyao husema na kufanya, kile ambacho katiba, Bunge na sheria zinasema kuhusu masuala ya kijamii na kisiasa, sera na matukio. Lakini ubepari, itikadi iliyo na umaarufu, ambayo inaweka mwelekeo wa matukio yote, mara chache huonekana wazi. Hata hivyo inaathiri maisha ya mamilioni ya watu.
Vile vile maisha na vifo vya wafanyikazi, watu na mapambano yao ya maisha katika mazingira ya uhasama wa kiuchumi, kisiasa na kijamii yaliyoundwa na ubepari yamefichwa kutoka kwa habari na ufahamu wa umma. Pia pingamizi yao kwa ubepari na mapambano ya kufanikisha usosholisti hayatokei katika rekodi rasmi.
Ubepari hutanda nyuma ya pazia, bila kuonekana wala kusikilizwa lakini bila kuchoka ili kuendesha ajenda yake fiche katika mwelekeo wa kiitikadi uliowekwa na kubainishwa ili kuushinda usosholisti kwa kuusifia ubepari na ubeberu ili uonekane kuwa bora. Mara nyingi, demokrasia ya uongo hutumika kudanganya watu na kueneza ajenda fiche ya ‘faida- binafsi-nzuri’. Kinachoonekana hadharani ni katiba, uchaguzi, mifumo ya bunge, vyama vya siasa na mfumo wa kisheria unaodhaniwa kuwa nguvu nyuma ya matukio.
Shinikizo muhimu zaidi katika kuamua hatima ya watu na nchi haijaonyeshwa katika vyombo vya habari vinavyodhibitiwa na kampuni, mifumo ya elimu, historia na sera za serikali. Ubepari basi pia huficha kutoka kwa umma athari mbaya ya utawala wake. Inaficha kuwepo kwake. Ubepari hauwezi kuonekana au kueleweka kwa kutengwa na usosholisti, ambo ni kinyume chake. Na kwa hivyo, usosholisti — itikadi yake, uwepo wake, udhihirisho wake na jina lake — pia umefichwa na tabaka za watawala. Hisia ya uwongo inaundwa kwamba ubepari ndio njia pekee inayoweza kuandaa jamii. Upinzani kwa ubepari unaonyeshwa kama vitendo vya watu wanaoongozwa na nia na nguvu za giza.
Ubepari hutwika mapungufu yake na migogoro inayowaletea wafanyikazi kwa mambo ya nje au kwa ‘nia mbovu’ ya watu ‘wabaya’, ‘magaidi’ na kusingizia dini, utaifa, jinsia, eneo au watu binafsi wanaounga mkono usosholisti — kamwe ubepari usionekane kuwa asili ya maovu haya. Ubepari unaenea sana katika kila nyanja ya Maisha, hivi kwamba kuwepo kwake hakuonekani. Uko kila mahali, lakini unaishi katika vivuli, na huendesha jamii, matukio na watu binafsi kutoka kwa udhibiti wa mawimbi ambao hauwezi kufuatiliwa kwa urahisi hadi kitovu chake.
Kipengele kingine kinachofichwa na ubepari ni mgawanyiko wa jamii katika matabaka pinzani ambayo ubepari wenyewe huyaunda. Suluhu yake kwa matatizo inayoibua ni ‘sote tupo ndani pamoja’ ilhali ni wazi kwamba tabaka tawala ziko mbali na ukweli wa maisha ya wafanyakazi. Ubepari hushambulia tabaka la wafanyakazi, mashirika yake — vyama vya wafanyakazi — na viongozi wao ili kunyamazisha upinzani. Pia mashambulizi yao yanalenga wakulima, wafugaji, wavuvi, pamoja na wataalamu wa maendeleo, wanafunzi na wanaharakati. Hivyo mabepari wanasafisha njia kwa unyakuzi wa mali ya taifa bila woga wa kupinduliwa.
Kipengele cha tatu ambacho kinafichwa na ubepari ni harakati zake za kutafuta faida binafsi bila kuchoka na ambazo zinazoendesha vitendo vyake vya uporaji, unyonyaji na ukandamizaji wa watu wanaofanya kazi. Chini ya ajenda yake ya ‘uhuru’, ubepari unabinafsisha huduma na taasisi za umma katika sera ya kufidia kila kitu. Kisha hutumia mamlaka yake ya serikali kuwatajirisha zaidi wasomi wanaotawala, mashirika na mtaji wa kifedha huku ikiwafanya watu wanaofanya kazi kulipia hizi huduma kwa njia mbalimbali zenye uharibifu. Ajenda zake zisizoonekana na zisizoandikwa huendesha matukio ambayo hufanywa yaonekane ‘ya kawaida’. Ubeberu, kwa msaada wake kwa tabaka tawala nchini Kenya, unahakikisha kwamba huo na ubepari unabaki bila kuonekana na kutotajwa hadharani. Bado unaipeleka nchi katika mwelekeo ambao unakidhi tu kiu chake cha faida kisichoisha. Unasimamia taasisi zote za kidemokrasia, mabunge, vyama vya siasa na hata Katiba kwa niaba yake. Unatumia nguvu za kiraia na kijeshi inazodhibiti ili kufikia ajenda yake inayotokana na faida. Inafuta kila kizuizi katika njia yake.
Tamaa ya faida basi inahitaji mashirika kudhibiti mawazo ya watu na ufahamu wa matukio ya kihistoria na ya sasa. Inatumia zana kadhaa ambazo imejinasia ili kudhibiti akili za watu. Hizi ni pamoja na vyombo vya habari, sera ya elimu, taasisi za habari kama vile maktaba ambazo zote zinafanywa kuakisi mtazamo wa kibepari katika kazi zao huku zikiwa na mkao wa kutoegemea upande wowote. Inashawishi idara za historia katika vyuo vikuu ili kusiwe na utafiti au mafundisho juu ya upinzani dhidi ya ubepari, historia ya Mau Mau, au vita vya uhuru wa Kenya. Upinzani dhidi ya ubepari na ubeberu ni sehemu zisizoweza kugusika na wasomi wala taasisi za ‘elimu ya juu’.
Na bado, upinzani wa watu dhidi ya ubepari na mapambano ya usosholisti sasa imekuwa sifa kuu ya maisha. Hii ni kweli si tu nchini Kenya, bali kote barani Afrika na, kwa hakika, katika ulimwengu ambapo ubepari daima hupata upinzani kwa ajenda yake ya unyonyaji na ukandamizaji isiyokoma. Katika harakati ya watu kutafuta usosholisti, ambao pekee unaweza kutoa haki na usawa wanaoutafuta, hakuna uchovu.
Ubepari unapokabiliwa na kuonegezeka kwa upinzani kutoka kwa watu, itikadi hiyo hutumia matukio kama vile coronavirus kurudisha nyuma faida ambazo watu wamepata kwa miongo kadhaa ya upinzani.
Katika wakati wa uhuru nchini Kenya, na kwa hakika katika nchi nyingi za Afrika, hapakuwa na suala la kuendeleza ubepari ambao ulikuwa umeanzishwa na ukoloni. Usosholisti ndio ulikuwa njia pekee mbele. Thomson (2010, uk.38) anatoa muhtasari wa kesi ya usosholisti:
Si jambo la kushangaza kwamba mataifa mengi barani humu yalichukua mtazamo wa kisoshalisti baada ya uhuru. Baada ya kuziondoa nchi zao katika utawala wa kikoloni, kazi sasa ilikuwa kupunguza utegemezi kwa nchi za Magharibi, na kurekebisha uchumi ili kuhakikisha kwamba mahitaji ya maendeleo ya ndani yanapewa kipaumbele. Ni kwa njia hii tu ndipo umaskini ungeweza kupungua na ustawi wa jamii kutolewa kwa wote.
Miongoni mwa viongozi wachache wa Kiafrika waliochukulia ubepari kuwa itikadi inayofaa kwa nchi ni Jomo Kenyatta. Haiwezi kusemwa kwamba chaguo lake lilijikita katika kuhakikisha kwamba mahitaji ya maendeleo ya ndani yanakidhiwa, mbali na kupewa kipaumbele. Kusudi lake linaonekana kuwa ulafi mtupu wa mali na madaraka kwa ajili yake mwenyewe, jamaa yake na wale waliomzunguka. Ubepari ndio ulikuwa chaguo pekee la kutimiza matamanio yake. Hata hivyo, haikuwezekana kutangaza kushikamana kwake na ubepari wakati watu na vyama vya kisiasa na urithi wa Mau Mau wakidai usosholisti. Kwa kuungwa mkono na ubeberu, Kenyatta na Tom Mboya, wafuasi wakuu wa itikadi za ubepari, walikita mizizi ubepari chini ya neno ‘Usosholisti wa Kiafrika‘ ambao haukuwa na uhusiano wowote na usosholisti au uAfrika. Ilikuwa ni mbinu ya kuficha jumuiya ya mbwa-kula-mbwa huku Kenyatta akiwa ndiye mwenye kunufaika zaidi. Ilizidisha migawanyiko ya kitabaka ambayo ilinufaisha wasomi waliokuwa wakitawala chini ya Kenyatta, na fedha na mashirika ya kimataifa, na kuwaacha watu wengi wakihangaika kutafuta maisha.
Kwa vile upinzani nchini Kenya ulilazimisha kufika kwa uhuru, Uingereza ililenga kuhakikisha kwamba Kenya inasalia kuwa ya kibepari na haigeukii usosholisti. Ilipindua malengo ya mapambano ya Mau Mau na jitihada yake ya kutafuta wa ardhi, uhuru na haki. Wenye itikadi kali katika Mau Mau na katika chama cha KANU walifahamu vyema hatari hii ya ukoloni mamboleo kama walivyoeleza mwaka wa 1961 katika hati yao ya Njia Mbili Mbele (1973).
Jomo Kenyatta kuwaunga mkono Waingereza kwa ushirikiano na watu aliowaongoza ulihakikisha kuwa ubepari na serikali yenye mwelekeo wa ubeberu inabaki madarakani. Msaada huu ulijumuisha kukandamizwa kwa vyama vya siasa kali, vyama vya wafanyakazi, mashirika ya kisiasa na kijamii, matumizi ya sheria za enzi za kikoloni dhidi ya watu pamoja na kutengwa na kudhoofishwa kwa viongozi waliokuwa tishio kwa utawala wao. Miongoni mwa wahasiriwa wa mapema ni Shujaa Pio Gama Pinto kuuawa mnamo 1965. Mbinu zingine zilizotumiwa kukuza maadili ya kibepari miongoni mwa vizazi vichanga ni pamoja na kutumia elimu, utamaduni, vyombo vya habari na sheria kama njia za kuunda Hakuna-Mbadala-Kwa-Mtazamo wa kibepari. Zawadi zilitolewa kwa ‘marafiki wa ubepari’ na adhabu kwa wale waliokataa itikadi hiyo. Uingiliaji huu wa kibeberu nchini Kenya ulihakikisha kuwepo kwa ubepari baada ya uhuru. Pia mawazo ya usosholisti yaliondolewa kutoka kwa fikra za umma. Lakini yaliendelea, wakati mwingine peupe, wakati mwingine kisiri.